Jumatano , 25th Nov , 2020

Michuano ya ligi ya mabingwa barani ulaya imeendelea usiku wa kuamkia hii leo kwa michezo nane ya mzunguko wa wanne vilabu vya Chelsea, Sevilla kutoka kundi H, FC Barcelona na Juventus kutoka kundi G vimefanikiwa kupata ushindi na kujihakikishia kutinga hatua ya 16 bora ya michuano hiyo.

Cristiano Ronaldo akishangilia bao katika mchezo walioshinda jana dhidi ya Ferencvaros.

Chelsea ndiyo ilikuwa timu ya kwanza kujihakikishia kufuzu hatua hiyo ya mtoano ya 16 bora baada ya mchezo wake dhidi ya Rennes ya Ufaransa kumalizika mapema kwa Cheslea kupata ushindi wa mabao 2-1 kwenye dimba la ugenini la Roazhon nchini Ufaransa.

Mabao ya Chelsea yamefungwa na mshambuliaji wa pembeni kinda Callum Hadson-Odoi aliyefunga dakika ya 22, mshambuliaji Sehrou Guirassy aliwasawazishia Rennes dakika tano kabla ya mchezo kumalizika lakini mshambuliaji Olivier Giroud aliibuka shujaa baada ya kufunga bao dakika za niongeza.

Sevilla ndiyo timu ya pili kufuzu kutinga hatua ya16 bora baada kuwanyuka krasnodar ya Urusi mabao 2-1, Kiungo mkongwe Ivan Rakitic akifunga dk2, Winga Wanderson akasawazisha dakika kumi tu akiingia kutokea benchi na hatimaye Munir El Hadad akafunga dakika za nyongeza na kuwavusha Sevilla.

Wawili hao kutoka kundi H wamefuzu Chelsea akiwa kinara na alama 10 sawa na Sevilla hivi sasa wameungana na FC Barcelona na Juventus ambao wamefuzu baada ya kupata ushindi ikiwa ni miongoni mwa michezo sita iliyoanzwa kucheza saa tano usiku na kumalizika usiku mnene.

FC Barcelona wameshika usukani wa kundi G wakifikisha alama 12 ikiwa ni ushindi wa 100% kwenye michezo minne ilhali hawakuwa na wachezaji wao nyota kama vile Lionel Messi, Ansu Fati, Sergi Roberto na Sergio Busquets wenye majeraha na wengine kupumzishwa na kocha Reonald Koeman.

Barcelona imeichabanga Dynamo Kyiv ya Ukraine iliyocheza bila wachezaji wake 9 wa kikosi cha kwanza mabao 4-0 ambayo mawili yamefungwa na Martin Braithwaite, moja na Sergino Dest na la nne likifungwa na Antoine Greizmann aliyetokea benchi.

Juventus ya CR7 imeifunga Ferencvaros ya Hungary mabao 2-1 CR7 akifunga moja na Alvaro Morata akitupia lingine wakati Myrto Uzuni akiweka kambani bao la kuwafuta machozi. Matokeo ya michezo mingine ni pamoja na Mashetani Wekundu Manchester United kumdunda Istanbul Basaksehir 4-0.

Kiungo fundi Bruno Fernandez akiweka kambani mabao 2, Rashford na Daniel James wakifunga bao moja moja na kuwabakisha Man utd kileleni mwa kundi H. PSG wamejitutmua na kuwafunga RB Leipzig kwa mbinde bao 1-0 lililofungwa kwa mkwaju wa penalti na Bishoo Neymar Junior dk ya 11.

Borussia Dortmund ya Ujerumani imeonesha ubabae kwa kuwanyuka Club Brugge ya Ubeligiji mabao 3-0 na nyota Erling Braut Halaand akiendelea kuibuka gumzo kwani amefumania nyavu mara 2 wakati Jadon Sancho akifunga bao moja na Dortmund kusalia kileleni mwa kundi F.

Lazio ya nchini Italia haijapoteza pambano, imewanyuka Zenit St.Petersburg mabao 3-1, Cirlo Immobile akiweka kambani mara mbili wakati Kiungo Marco Parolo akiweka moja, Artem Dzyuba akifunga moja la kufutia machozi vijana wa Putin.

Michezo ya ligi ya mabingwa barani ulaya inatazamiwa kuendelea kuchezwa kuanzia usiku wa hii leo kwa michezo nane ya kukamilisha mzunguko wa nne huku michezo miwili ikianza kuchezwa mapema saa mbili na dakika hamsini na tano za usiku kwa saa za Afrika ya Mashariki.

Vinara wa kundi B klabu ya Borussia Moenchengladbach watajitupa dimbani kupepetana na Shakhtar Doneskt ya Ukraine usiku wa saa mbili na dakika hamsini na tano wakati huo huo kunako kundi C, Olympiacos ya Ugiriki watawavaa Manchester City ambao watafukuzu endapo wakishinda.

Michezo sita iliyosalia inatarajiwa kuchezwa saa tano kamili usiku wa hii leo ambapo kigogo klabu ya Bayern Munich kutoka kundi A watajihakikishia kufuzu endapo wakipata ushindi mbele ya wabishi wa Austria klabu ya Salzburg, Atletico Madrid dhidi ya Locomotive Moscow ya Urusi.

Kwenye kundi D lenye bingwa mtetezi Liverpool, ambao hii leo watapapatuana na Atalanta kutoka Italia na endapo watashinda hii leo basi watajihakikishia nafasi ya kufuzu kutinga hatua ya mtoano ya 16 bora ya michuano hiyo wakati Ajax watacheza dhidi ya Midtjylland ya Denmark.