Jumatano , 15th Nov , 2017

Klabu ya  ya Mbeya City inayoshirki ligi kuu soka Tanzania bara leo inatarajia kushuka dimbani kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Coastal Union kwenye uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Meneja wa Mbeya City, Geoffrey Katepa amesema mchezo wa leo ni sehemu ya maandalizi ya mchezo wao wa ligi kuu dhidi ya Yanga kwenye uwanja wa Uhuru jiji Dar es salaam.

Katepa ameeleza kuwa timu imefika jijini Tanga jana usiku kwaajili ya kambi ya muda mfupi ambapo itacheza mchezo wa leo na Coastal Union ambayo inashiriki ligi soka daraja la kwanza.

Baada ya mchezo wa leo timu  itaendelea na mazoezi hadi siku ya ijumaa ambapo itasafiri kwenda jijini  Dar es Salaam tayari kuwavaa mabingwa watetezi Yanga kwenye mchezo wa raundi ya 11 Jumapili hii.

Baada ya kupisha mechi za kirafiki za kalenda ya FIFA ligi kuu soka Tanzania bara inarejea wikiendi hii kwa michezo kadhaa kupigwa ukiwemo ule wa Jumamosi ambapo Azam FC itakuwa mgeni wa Njombe Mji FC wakati vinara wa ligi hiyo Simba SC watakuwa jijini Mbeya kukabiliana na Tanzania Prisons.