Jumanne , 28th Mar , 2017

Mshambuliaji chipukizi kutoka klabu ya Kagera Sugar inayoshiriki ligi kuu Tanzania Bara, Mbaraka Yusuph hii leo amejiwekea rekodi ya kipekee mara baada ya kuifungia bao la ushindi Taifa Stars iliyokuwa inakipiga na timu ya taifa ya Burundi

Mbaraka Yusuph

Katika mchezo huo Taifa Stars imeibuka na ushindi wa mabao 2-1, ambapo Mbaraka amefunga bao la pili kwa juhudi binafsi baada ya kutengenezewa mpira na Said Ndemla katika dakika ya 76 ya mchezo ikiwa ni takriban dakika 5 tangu aingie kuchukua nafasi ya Farid Musa akitokea benchi.

Kijana huyu ambaye ni miongoni mwa wafungaji watano wanaoongoza kwa mabao mengi katika ligi kuu Tanzania Bara akiwa na mabao kumi, hii ni mara yake ya kwanza kuitwa Taifa Stars na kupata nafasi ya kucheza, ambapo katika dakika takriban 20 ameweza kufungua akaunti ya mabao kwa kupachika bao lake la kwanza na ambalo ni la ushindi.

Katika ligi kuu, Mbaraka ana mabao 10 nyuma ya Tambwe, Kichuya na Msuva mwenye mabao 12, na huenda siku ya leo ikawa ya kihistoria kwake kwa kuwa ndiyo mara ya kwanza anavaa jezi ya Taifa Stars na kupachika bao la ushindi.

Katika mchezo wa leo ambao Taifa Stars ilimkosa nahodha wake Mbwana Samatta, imeonesha soka la ushindani na kufanikiwa kupata bao la kwanza katika dakika ya 20 kupitia kwa Saimon Msuva aliyeunganisha moja kwa moja kwa shuti kali kros ya Mohamed Hussein.

Burundi wamepata bao lao dakika ya 53, kupitia kwa Laudit Mavugo aliyetumia vizuri makosa ya beki wa kati wa Taifa Stars Abdi Banda aliyeshindwa kutuliza mpira katika eneo la hatari mpira ambao ulimkuta Mavugo akiwa kwenye nafasi na kmtundika kipa wa Stars, Dida.

Wachezaji wa Burundi wakishangilia bao

Mabadiliko yaliyofanyika katika mchezo wa leo ni pamoja na kuwatoa Sure Boy na kuingia Ndemla, Jonas Mkude aliingia kuchukua nafasi ya Ajibu aliyeumia, Kichuya alichukua nafasi ya Mzamiru na Mbaraka alichukua nafasi ya Farid.

Kikosi cha kilichoanza katika mchezo wa leo ni hiki

Huu ni ushindi wa pili mfululizo kwa Taifa Stars katika michezo hii ya kirafiki iliyo chini ya kalenda ya FIFA