Jumanne , 25th Jul , 2017

Mshambuliaji wa timu ya Taifa ya Tanzania, Mbaraka Yusuph amethibitisha kwamba kwa sasa yeye ni mchezaji wa Azam Fc ambayo imemsajili mara baada ya kumalizika kwa msimu uliopita na pia hana mkataba na Kagera Sugar kama inavyozungumzwa.

"Siyo kila anayekwenda TFF anakesi mimi mkataba wangu wa Kagera umekwisha salama na tayari nimesaini na Azam FC hivyo ni kitu kikubwa kwangu na wala hakuna migogoro nyuma yangu" amesema kwenye mahojiano na EATV

Mbali na hayo Mbaraka ambaye alitikisa vilivyo msimu uliopita kwa kuviadhibu vilabu vya Yanga na Simba amesema kuitwa katika kikosi cha Stars kumemjengea imani kubwa kuwa anaweza kufanya chochote katika soka na kwa sasa inambidi apambane zaidi ili aweze kutimiza ndoto za kucheza soka la kulipwa.

Nyota huyo ambaye alikulia katika klabu ya Simba kabla ya kutolewa kwa mkopo Kagera Sugar na kuuzwa moja kwa moja amesema nidhamu na kujituma ndio nguzo pekee ya mchezaji yoyote mwenye malengo ya kufanikiwa kupitia mchezo huo.

Kinda huyo tegemeo la Tanzania amewaasa chipukizi kuwa wavumilivu na kujituma ili waweze kufika mbali katika medali ya soka kama anavyoona kwa upande wake hivi sasa.

Pamoja na hayo Mbaraka amedai kuwa  kuwepo kwake katika timu ya Taifa kumemfanya aweze kuanza kutimiza ndoto zake alitokua akiziota tangu utotoni kwa kucheza soka katika kiwango cha mbali zaidi.