Jumatano , 15th Nov , 2017

Kocha wa klabu ya Lipuli FC Suleiman Matola amesema tayari ameshawasilisha kwa uongozi mahitaji ya wachezaji anaowahitaji kwenye dirisha dogo la usajili.

Matola amesema kikosi chake kina mapungufu kwenye safu ya ushambulijai hivyo ni lazima afanye usajili kwenye dirisha dogo ili kuboresha timu yake kwaajili mwendelezo wa michezo ya ligi kuu.

Kwa upande wa idadi ya wachezaji Matola ameeleza kuwa anahitaji wachezaji wanne ili kukamilisha mipango yake ya kupata matokeo mazuri.

“Timu yangu inahitaji wachezaji wanne wakiwemo washambuliaji eneo ambalo mimi naona bado lina upungufu lakini pia maeneo mengine ikiwemo kiungo na ulinzi”, amesema Matola.

Matola amesema ana matumaini kuwa mapendekezo yake yatafanyiwa kazi mapema na uongozi wa klabu hiyo ambayo imepanda daraja msimu huu. Lipuli FC inashika nafasi ya 7 ikiwa na alama 14.

Dirisha dogo la usajili kwa vilabu vya ligi kuu Tanzania Bara limefunguliwa rasmi leo Novemba 15 na litadumu kwa kipindi kifupi cha mwezi mmoja kabla ya kufungwa Desemba 15 mwaka huu.