Jumanne , 24th Nov , 2020

Uongozi wa klabu ya Yanga umethibitisha ya kuwa rasimu ya kwanza ya mchakato wa mabadiliko ya uendeshwaji kwenye klabu hiyo imekamilika na wanasubiri wasaa ufike ili waendelee na rasimu ya pili ya mchakato huo.

Mkurugenzi wa uwekezaji wa GSM, Hersi Said( kulia) na Alvaro Paya ambaye ni mwakilishi wa La liga (Kushoto) kwa pamoja wakiwa uwanja wa ndege wa JK tayari kwa safari ya kuelekea Hispania.

Yanga wameyasema hayo kupitia mshauri mkuu wa klabu hiyo Senzo Mazingisa wakati akizungumza na wanahabari kwenye makao makuu ya klabu hiyo na kuweka wazi safari ya kwenda nchini Uhispania kufuata ripoti ya kukamilika kwa rasimu ya kwanza imewadia.

Mkurugenzi wa uwekezaji kutoka GSM kwenye klabu ya Yanga Hersi Said na mwakilishi wa La Liga Alvaro Paya wamesafiri usiku wa kuamkia hii leo kuelekea nchini Hispania kukabidhiwa ripoti ya rasimu ya kwanza ya mchakato wa mabadiliko ya uendeshwaji kutoka mfumo wa uanachama kuwa kampuni ya mfumo wa umiliki hisa.

Hersi ameelekea nchini Hispania kupokea ripoti hiyo kutoka kwa maafisa wawakilishi kutoka ligi kuu nchini humo 'La liga' ambao wana makubaliano ya kimkataba kusimamia na kuwasaidia Yanga kufanya mabadiliko hayo kwa ueledi na usasa mkubwa kwa manufaa ya soko la kibiashara katika soka.

Baada ya Yanga kupokea ripoti hiyo watapata ufafanuzi kutoka kwa maafisa wa La Liga na kurejea na ripoti nchini na kisa kuwajuza wanachama na wapenzi wa Yanga maana ya ripoti hiyo na kufafanua zaidi hatua waliyofikia katika kuelekea mabadiliko hayo.