Jumanne , 26th Jan , 2021

Mlinzi nyota wa Los Angeles Clippers, Kawhi Leonards ataukosa mchezo dhidi ya Atlanta Hawks wa NBA utakaochezwa saa 9:30 alfajiri ya kuamkia kesho Januari 27, 2021 kufuatia taratibu mpya za kujikinga na Covid-19 kumfanya ashindwe kujiunga na timu yake.

Mlinzi nyota wa LA Clippers, Kawhi Leonards.

Leonards analazimika kusubiri vipimo vya mwisho vitakavyotoa majibu juu ya Afya yake ukiwa ni utaratibu mpya kwenye ligi hiyo ya kikapu nchini Marekani NBA unaomtaka kila mchezaji, kocha na wahusika wa karibu na mchezo kupimwa Afya kabla ya kila mchezo.

Clippers imethibitisha pia kuwakosa nyota wake wengine wawili, mlinzi Patrick Beverley mwenye maumivu ya goti na Paul George mwenye maumivu ya misuli yaliyomfanya ashindwe kumaliza mchezo uliopita dhidi ya Oklahoma City Thunder waliopata ushindi wa alama 108 kwa 100 jumapili iliyopita. 

(Mlinzi wa LA Clippers, Patrick Beverley)

Taarifa za Kawhi Leonards na George kujiunga na msafara wa timu ya LA Clippers kuelekea mchezo wao unaofuata bado hazijawekwa wazi kwasababu bado nyota hao wapo kwenye uangalizi wa madaktari.

(Mlinzi wa LA Clippers, Paul George)

Kama Clippers itafanikiwa kupata ushindi alfajiri ya kesho basi watakuwa wanafukuzuia rekodi ya kucheza michezo saba bila kufungwa na kuzidi kuwapa presha wapinzani wao Los Angeles Lakers ambao ndiyo mabingwa watetezi na vinara wa Western Conference.

Hivi sasa LA Clippers ipo nafasi ya pili baada ya kushinda michezo 13 na kupoteza mmoja ilhali vinara LA Lakers wameshinda michezo 14 na kufungwa 4 na kuwa mbele kwa mchezo mmoja.