Jumamosi , 15th Mei , 2021

Wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya klabu bingwa barani Afrika Simba SC watatupa karata yao ya kwanza leo usiku kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza wa hatua ya robo fainali dhidi ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, mchezo huu unachezwa katika dimba la FNB Afrika Kusini.

Wachezaji wa Simba SC

Ushindi wa michezo minne sare ya mchezo mmoja na kupoteza mchezo mmoja ilitosha kuipa Simba alama 13 na kumaliza vinara wa kundi A' na leo wataminyana na Kaizer Chiefs ambao walimaliza nafasi ya pili kwenye kundi C' kwa jumla ya alama 9.

Wenyeji wa Kaizer Chiefs wamekuwa na rekodi nzuri katika uwanja wa nyumbani, katika hatua ya makundi hawajapoteza mchezo hata mmoja kwenye dimba la FNB wameshinda michezo miwili na wametoka sare mchezo mmoja na hawajaruhusu bao hata moja kwenye dimba hilo.

Wakati rekodi za Simba ugenini pia sio mbaya wameshinda mchezo mmoja tu ugenini wakipata sare mchezo mmoja na wamefungwa mchezo mmoja, lakini pia wekundu wa msimbazi wamefungwa bao 1 tu kwenye michezo mitatu ya hatua ya makundi waliocheza ugenini.

Simba hawana mchezaji mwenye majeruhi au mwenye adhabu atakayeukosa mchezo wa leo usiku wachezaji wote waliosafiri wapo tayri kwa mchezo ni uamuzi tu wa kocha Didier Gomez Da Rosa, kwa upande wa Kaize mshambuliaji wao Samir Nurkovic atakuwa akirejea baada ya kumaliza kutumikia adhabu, lakini wataendelea kumkosa golikipa wao Daniel Akpeyi ambaye anatumikia adhabu, Khama Billiat na mlinzi Mathoho bado wana majeruhi.