Jumatatu , 28th Sep , 2020

Msimu wa 2020/21 kwa Vilabu Barani Ulaya umeendelea kwa kasi huku wiki iliyopita matukio mbali mbali yalijitokeza mengine yakiwa ya kushtusha kulingana na matokeo yaliyojitokeza.

Cristiano Ronaldo akiukokota mpira wakati Juventus ilipokua ikikabiliana na AS Roma kwenye mchezo wa Serie A uliomalizika kwa sare ya bao 2-2.

Leicester City ilikuwa klabu ya kwanza kufunga magoli matano katika mchezo mmoja dhidi yaTimu inayofundishwa na kocha Pep Guardiola, baada ya kupata ushindi wa 5-2 katika mchezo uliopigwa kwenye dimba la Etihad.

Hii ilikua ni hat trick ya pili kwa Jamie Vardy kuifunga City kwani Desemba 10, 2016 alifunga tena wakati Leicester City ikishinda 4-2 dhidi ya wababe hao wa jiji la Manchester.

Jamie ameweka rekodi ya pekee ya kuzifunga bao 35 timu kubwa sita (Arsenal, Liverpool, Man City,Manchester United, Tottenham Hotspurs na Chelsea) kwenye EPL.

Wakati Atletico Madrid inapata ushindi wa mabao 6-1 dhidi ya Granada kwenye mtanange wa La liga, Mshambuliaji mpya wa timu hiyo Luis Suarez alifunga mabao 2 na kutoa pasi 1 ya bao ndani ya dakika 24 tuu alizocheza, huku ikiwa ni mchezo wake wa kwanza toka ajiunge na miamba hiyo ya Madrid.

Hivyo sasa Suarez amefikisha mabao 319 tangu aanze kucheza soka la kulipwa.

Kinda wa Barcelona akiwa na miaka 17 alifanikiwa kupachika mabao 2 ndani ya dakika 19 wakati Barca ikiiichapa Villareal kwenye dimba la Camp Nou.

Tangu Ansu apandishwe kwenye timu ya wakubwa amefunga mabao 9 katika michezo 25 aliyocheza.

Mlinzi wa Real Madrid, Sergio Ramos alifunga bao dhidi ya Real Betis wakati timu yake ikiibuka kidedea na ushindi wa magoli 3-2, na kumfanya afikishe mabao 71 katika mechi 456 alizocheza akiwa Los Blancos.

Nchini Italia Juventus ilipata sare ya bao 2-2 dhidi ya AS Roma lakini Mshambuliaji hatari wa kibibi kizee hicho, Cristiano Ronaldo alifunga mabao 2 na kupelekea kufikisha magoli 450 kwenye ligi tatu kubwa alizocheza mpaka sasa.

Napoli nayo ilishusha kipigo kizito cha mabao 6- 1 dhidi ya Genoa huku bao moja wapo likifungwa na Mshambuliaji tegemezi Dries Mertens ambae sasa amefikisha mabao 95 katika michezo 238 tangu ajiunge na klabu hiyo 2013 akitokea PSV ya Uholanzi.

AC Milan nayo ilishinda mchezo wa pili mfululizo katika Serie A msimu huu, ambapo iliinyuka Crotone mabao 2-0.

Inter Milan nayo ilianza vyema msimu kwa ushindi wa mabao 4-3 dhidi ya Fiorentina huku goli moja wapo likifungwa na Mbelgiji Romeru Lukaku ambaye amefikisha mabao 3 katika mechi 52 alizoichezea Milan.

Nchini Ujerumani, mabingwa watetezi wa Bundesliga, Bayern Munich ilipokea kipigo cha kwanza cha goli 4-1 kutoka kwa TSG Hoffenheim , mara baada ya kushinda michezo 23 mfululizo na pia kutopoteza mchezo wowote katika mechi 32 zilizopita.