Jumapili , 19th Feb , 2017

Azam FC, leo inashuka tena dimbani kuvaana na Mwadui FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara (VPL) utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam saa 1.00 usiku.

Azam na Mwadui

Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi msimu huu, wamejipanga kuhakikisha wanazoa pointi zote tatu ili kuzidi kujiongezea pointi, ambapo mpaka sasa imejikusanyia 38 katika nafasi ya tatu nyuma ya pointi 13 dhidi ya kinara Simba aliyejikusanyia 51.

Azam iliichapa timu hiyo mabao 4-1 katika mchezo wa raundi ya kwanza uliofanyika mkoani Shinyanga na mchezo wa leo utakuwa ni wa nne kwa Azam FC kucheza na Mwadui katika ligi tangu timu hiyo ipande daraja, ambapo imeifunga mara zote ikiwa imetupia mabao sita na kuruhusu wavu wake kuguswa mara moja pekee.

Mbali na mechi ya ligi, timu hizo zimewahi kukutana kwenye nusu fainali ya Kombe la Shirikisho na Azam FC ikashinda kwa mikwaju ya penalti 5-3 kufuatia ndani ya dakika 120 za mchezo huo timu hizo kutoka sare ya mabao 2-2.

Pia walitoka sare ya bao 1-1 katika mchezo wa kirafiki wa kujiandaa na msimu uliopita uliofanyika Uwanja wa Azam Complex.

Azam FC itaendelea kuwakosa wachezaji wawili nahodha John Bocco ‘Adebayor’ na kiungo Stephan Kingue, ambao bado wanauguza majeraha yao ya misuli ya nyama za paja, lakini itakuwa na urejeo wa kiungo Salum Abubakar, aliyepona maumivu ya mguu yaliyokuwa yakimkabili.