Ijumaa , 21st Apr , 2017

Hatimaye shauku ya wadau wa soka imekwisha baada ya Chama cha Soka barani Ulaya (UEFA) leo kuweka wazi ratiba kamili ya michezo ya nusu fainali katika michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya pamoja na 'Europa League'

Katika droo iliyofanyika leo, mahasimu wa soka katika jiji la Madrid nchini Hispania, Real Madrid na Atletico Madrid wamekutanishwa kwa mara nyingine tena, baada ya kukutana katika fainali ya msimu uliopita, ambapo Real Madrid walitwaa ubingwa kwa mikwaju ya penati.

Real Madrid wanaanzia nyumbani siku ya tarehe 2 mwezi Mei na kurudiana siku ya tarehe 9.

Nusu fainali ya pili inawakutanisha Wafaransa AS Monaco ambao ni wanafainali wa mwaka 2003, Monaco dhidi ya Juventus ambao pia ni wanafainali wa mwaka 2015 siku ya tarehe 3 mwezi Mei mwaka huu.

Real imefikia hatua hiyo baada ya kuitoa Bayern Munich, Atletico imeitoa Leicester City, Monaco imeiondosha Borussia Dortmun na Juve imeisambaratisha vigogo FC barcelona.

Kwa upande wa nusu fainali ya Ligi ya Europa Mashetani wenkundu wa England Manchester United wamepelekwa Ufaransa kuikabili Celta Vigo, huku Wadachi Ajax wakianzia nyumbani dhidi ya Wafaransa wengine, Olimpique Lyon, mechi zote zikipigwa Mei 4 mwaka huu.

Man Unite iliitoa Anderlecht ya Ubeligiji kwa jumla ya mabao 3-2 huku Celta Vigo ikiiondosha Genk ya Ubelgiji pia ambayo anakipiga Mtanzania Mbwana Samatta kwa jumla ya mabao 4-3 katika hatua ya robo fainali.