Jumapili , 23rd Apr , 2017

Timu ya taifa ya Tanzania vijana wenye umri chini ya miaka 17 'Serengeti Boys'  jana walifanikiwa kuichakaza Gabon kwa mabao 2-1 kwenye mchezo wa kirafiki uliofanyika Rabat, nchini Morocco.

Serengeti Boys

Serengeti Boys imeweka kambi  Morocco kwa maandalizi ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17, zinazotarajiwa kuanza Mei 14 hadi 28 nchini Gabon. Katika mchezo huo mabao ya Serengeti yalifungwa na Kelvin Naftali na Ibrahim Ally.

Huo unakuwa mchezo wa nne wa maandalizi kwa Serengeti kujiandaa fainali za Gabon, baada ya kuifunga Burundi mara mbili na kulazimishwa sare ya 2-2 na Ghana ‘Black Starlets’. Mei 7 timu hiyo itakwenda Gabon ambako imepangwa kundi B pamoja na timu za Mali, Niger na Angola, wakati Kundi A lina timu za wenyeji, Gabon, Guinea, Cameroon na Ghana.