Jumatatu , 13th Nov , 2017

Bingwa mara sita wa fainali za dunia za ATP Roger Federer, ameanza vizuri fainali za ATP zilizoanza jana jijini London baada ya kumtupa nje Jack Sock.

Federer raia wa Uswis mwenye miaka 36, amecheza mchezo wake wa 15 msimu huu akifungua fainali hizo kwa ushindi wa seti 6-4 7-6 (7-4) kwenye uwanja wa O2 London.

Sock ambaye ni raia wa Marekani alikuwa anacheza fainali zake za kwanza za ATP akiwa amepata tiketi hiyo baada ya kushinda michuano ya Paris Masters wiki iliyopita.

Katika mchezo mwingine, Mjerumani Alexander Zverev amemshinda Marin Cilic raia wa Croatia kwa seti 4-6 6-3 6-4.

Michezo ya fainali hizo inaendelea leo ambapo Dominic Thiem atakwaana na Grigor Dmitrov, wakati mchezaji namba moja duniani Rafael Nadal atakipiga dhidi ya David Goffin, huku Jamie Murray akipambana na Bruno Soares.

Fainali za mwaka huu zinawakosa nyota kadhaa akiwemo bingwa mtetezi Andy Murray, bingwa mara tano Novak Djokovic na bingwa wa Grand Slam Stan Wawrinka ambao wote wanasumbuliwa na majeraha.