Jumapili , 19th Nov , 2017

Mshambuliaji wa Yanga raia wa Zambia Obrey Chirwa ameibuka shujaa kwenye mchezo wa ligi kuu raundi ya 10 dhidi ya Mbeya City baada ya kufunga mabao matatu kwenye ushindi wa mabao 5-0 leo jioni.

Katika mchezo huo Yanga imefanikiwa kuchukua pointi tatu kupitia mabao ya Obrey Chirwa na Emanuel Martin na kufikisha alama 20 nyuma ya Simba yenye alama 22.

Chirwa alifungua ukurasa huo wa mabao dakika ya 19 kipindi cha kwanza, kabla ya Emanuel Martin kuongeza bao la pili dakika ya 23. Mabao hayo yalidumu hadi mapumziko.

Kipindi cha pili Obrey Chirwa aliongeza bao la pili na tatu katika dakika za 50 na 59, wakati Emanuel Martin akizamisha jahazi la Mbeya City kwa kufunga bao la 5 na la pili kwake katika mchezo wa leo dakika ya 80.

Yanga sasa inashika nafasi ya tatu nyuma ya Azam FC na Simba zenye alama 22 kila mmoja zikitofautiana idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.