Jumanne , 27th Jun , 2017

Beki wa Kulia wa Klabu ya Simba aliyekuwa akiitumikia Klabu ya Azam FC Shomary Kapombe amewataka mashabiki kuendelea kumpa sapoti katika msimu ujao wa Ligi kuu ya Soka Tanzania Bara.

Kapombe amesema anaamini kutakuwa na ushindani mkubwa ndani ya Klabu ya Simba ambayo alishaitumikia kabla ya kujiunga na Azam FC lakini anaamini changamoto hizo zitamfanya kuwa mchezaji bora zaidi na kuweza kukuza kipaji chake.

“Unajua kufanya maamuzi kama nilivyofanya mimi inatakiwa kuwa na ujasiri, kwani sisi wachezaji tunakuwa na wakati mgumu sana katika kufanya maamuzi kipindi hiki cha usajili, nimetoka Azam FC na kulikuwa na changamoto kubwa ndani na nje ya Klabu, kwa sasa narejea tena Simba na nilianza kuifuatilia tangia msimu uliopita, nilikuwa naiona na naendelea kuiona kwani inawachezaji na benchi la ufundi zuri na naona kunachangamoto kubwa pia ambayo zitanifanya mimi kuendelea kuwa mchezaji mzuri, ” amesema.

“Naamini kiwango changu na ndoto zangu zitaendelea kuwa juu kwani nakutana tena na wachezaji wazuri kama nilipotoka na najua kutakuwa na ushindani mkubwa sana wa namba kwahiyo nimejiandaa na nachukulia changamoto nitakazokutana nazo ndizo zitanipa mafanikio zaidi, ” Kapombe aliongeza.

Shomary amewashukuru uongozi pamoja na mashabiki wa Azam FC kwakuwa naye pamoja na kukiboresha kikosi chake kwa muda wote aliokuwa nao.

“Naushukuru uongozi na mashabiki wa Azam FC kwani najua mchango wao kwangu pia mengi mazuri waliyonitendea, na hapa nilipofikia ni kwa ajili ya Azam FC kwani wamekiwezesha kipaji changu kufikia hapa na naamini nitafika mbali zaidi, ” amesema.

Shomary Kapombe aliitumikia Klabu ya Azam FC kwa miaka mitatu akitokea AS Cannes ambayo alienda akitokea Simba SC na sasa amerudi tena katika Klabu ya Simba kwa mkataba wa miaka miwili.