Ijumaa , 9th Apr , 2021

Kaimu kocha mkuu wa klabu ya Yanga, Juma Mwambusi amethibitisha kuwa watawakosa nyota wanne kuelekea mchezo wa ligi kuu soka Tanzania bara kesho Aprili 10, 2021 dhidi ya KMC, utakaochezwa saa 1:00 usiku kwenye dimba la Mkapa.

Nyota wa Yanga, Carlinhos Carmo atakayeukosa mchezo wa kesho dhidi ya KMC kutokana na kuwa na adhabu ya kadi nyekundu.

Wachezaji watakaokosekana ni viungo Haruna Niyonzima aliyewasili nchini jana akitokea kwenye kambi ya timu yake ya taifa ya Rwanda, Carlinhos anayetumikia adhabu ya kuoneshwa kadi nyekundu wakati Mapinduzi Balama na Mlinzi wa kushoto Yassin Mustapha wanauguza majeraha yao.

Pia amethibitisha kuwa mshambuliaji Said Ntibazonkiza amerejea kikosini baada ya kuwa nje kutokana na majeraha.

Ligi kuu soka Tanzania imerejea katika mwendelezo wake ambapo Yanga itakuwa inacheza mchezo wake wa 24 ikiwa inaongoza ligi kwa pointi 50. KMC wao wapo nafasi ya 5 wakiwa na pointi 35 kwenye mechi 24.