Jumatatu , 20th Nov , 2017

Mcheza tenisi Grigor Dimitrov raia wa Bulgaria ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kushinda taji la fainali za ATP kwenye mashindano yake ya kwanza kushiriki baada ya usiku wa kuamkia leo kumshinda David Goffin wa Ubelgiji.

Katika fainali hiyo Dimitrov, mwenye umri wa miaka 26, amefanikiwa kushinda taji lake kubwa la kwanza baada ya kushinda kwa seti 7-5 4-6 6-3 kwenye uwanja wa O2 jijini London.

Dimitrov ameshinda mechi zake zote tano alicheza kwenye fainali hizo kuanzia hatua ya makundi hadi fainali yenyewe na kufikia rekodi ya Mhispania Alex Corretja, ambaye naye alitwaa ubingwa huo kwenye mashindano yake ya kwanza mwaka 1998.

Dimitrov amesema haamini kile kilichotokea na hakumbuki alifanyaje kushinda fainali hizo ambazo hukusanya magwiji wa tenisi duniani ambapo msimu huu walikuwepo nyota kama Roger Federer na Rafael Nadal.

Pamoja na mafanikio hayo lakini nyota huyo amesema malengo yake makuu ni kushinda taji la Grand Slam hivyo ataendelea kuweka jitihada kuhakikisha anatimiza malengo hayo.