Jumatano , 29th Mar , 2017

Beki wa kati wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Aggrey Morris ameanza rasmi kufanya mazoezi mepesi baada ya kupata nafuu ya majeraha yake ya mfupa wa paja la kulia.

Aggrey Morris

Morris alipata majeraha hayo wakati Azam FC ikiichapa Mbabane Swallows bao 1-0 katika mchezo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika, ambapo katikati ya wiki iliyopita alianza na programu ya mazoezi ya ‘gym’ kabla ya kuhamia uwanjani.

“Nashukuru Mungu kwa kuweza kurejea uwanjani kwani lengo langu ni kucheza  na siyo kukaa nje ya uwanja kwa muda mrefu kwani hakuna kitu kibaya kwa mchezaji kama kupata majeraha yatakayomuweka nje ya uwanja kipindi kirefu sana” Alisema Morris

Beki huyo amerejea wakati Azam FC ikiwa kwenye maandalizi ya mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Yanga, utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wikiend hii (Jumamosi) majira ya saa 10.00 jioni.