Alhamisi , 26th Nov , 2020

Bingwa mtetezi wa kombe la ligi ya mabingwa barani ulaya, Bayern Munich ya Ujerumani ameanza vizuri safari yake ya kutetea taji hilo kwa kufanikiwa kutinga hatua ya mtoano ya 16 bora ya michuano ya ulaya baada ya kuichabanga klabu ya Salburg ya Austria mabao 3-1 usiku wa hapo jana.

Mshambuliaji wa Bayern Munich, Robert Lewandowski akishangilia bao alipofunga katika usiku wa Ulaya.

Mabao ya Bayern yamefungwa na Robert Lewandowski dakika ya 43, Kingsley Coman dakika 52 na Leroy Sane wakati lile la kufutia machozi ya Salzburg limefungwa na Mergim Berisha. Bayern amefuzu akiwa kinara wa kundi A na kushinda michezo yake yote minne na kujizolea alama 12.

Mchezaji bora wa michuano ya UEFA kwa msimu uliopita Robert Lewandowski mpaka hivi sasa amefikisha jumla ya mabao 14 na kutengeneza nafasi 5 za mabao katika michezo 13 kwenye michuano yote msimu huu.

Manchester City ya Uingereza wameungana na Bayern kwenye kufuzu hatua ya 16 bora licha ya ushindi mwembamba wa bao moja kwa sifuri lililofungwa na Phil Foden dakika ya 36 dhidi ya Olympiacos ya Ugiriki na kusalia usukani kwa kushinda michezo yake yote minne na kupata alama 12.

Ni mara ya nane mfululizo Man City kutinga hatua ya mtoano ya michuano hiyo huku wakiwa hawajafungwa kwenye michezo 15 ya makundi.

Kwa Upande mwingine, kocha wa City Guadiola amefurahishwa na wachezaji wake nyota Sergio Aguero na Fernandinho kurejea wakiwa fiti.

Kwa Upande wa Liverpool, Majogoo wa jiji wamepoteza mchezo wakiwa kwenye dimba lao la nyumbani 'Anfield' kwa mabao 2-0 dhidi ya Atalanta ya Italia.

Baada ya kipigo hicho Liverpool sasa wanalazimika kusaka alama tatu kwenye mchezo wao ujao ili kujihakikishia kufuzu hatua ya 16 bora.

Real Madrid ya Zinedine Zidane imewaduwaza wengi baada ya kuifunga Inter Milan ugenini kwenye dimba la Guisseppe di meaza mabao 2-0 ambayo yamefungwa na Eden Hazard kwa penalti dakika ya 7 kabla ya Artulo Vidal kuoneshwa kadi nyekundu dk ya 33 na baadaye Achraf Hakimi akajifunga dk59.

Los Blancos imepanda na kushika nafasi ya pili kwenye msimamo huo wa kundi B kwa tofauti ya alama 1 nyuma ya kinara wa kundi hilo Borussia Moenchengladbach, Shakhtar Donestk ya Ukrain wakiwa watatu wenye alama 4 wakati Inter Milan ya Italia wakishika mkia wakiwa na alama 2.

Orodha ya Vilabu vilivyofuzu hatua ya 16 bora ya michuano ya ligi ya mabingwa barani ulaya sasa imefika 6, Chelsea na Man City za Uingereza, Sevilla na Barcelona za Uhispania, Bayern Munich ya Ujerumani na Juventus ya Italia vikiwasubiri Liverpool na Man Utd ambao wanasaka alama moja.

Matokeo ya Michezo mingine iliyochezwa usiku wa hapo jana ni pamoja na Atletico Madrid kutoka suluhu na Lokomotiv Moscow, Merseille 0-2 FC Porto, Ajax 3-1 Midttjylland na Borussia Moenchengladbach 0-4 Shakhtar Donestk.