Jumatatu , 23rd Nov , 2020

Hemed Morroco, Kocha Mkuu wa Namungo FC amesema kuwa wachezaji wake walipambana kusaka matokeo uwanjani hivyo wanastahili pongezi licha ya kuambulia pointi moja walipokuwa Uwanja wa Mkapa.

Wachezaji wa Yanga na Namungo wakizozana katika mchezo wa jana wa VPL uliomalizika kwa sare ya bao 1-1.

Mchezo wa kwanza kwa Morroco kukaa kwenye benchi ilikuwa ni dhidi ya Yanga, Novemba 22 kwa kuwa alipokea mikoba ya Hitimana Thiery ambaye alifutwa Novemba 18 kutokana na mwendo mbovu wa timu yake.

Yanga ilianza kushinda kwenye mchezo huo dakika ya 13 kupitia kwa Carlos Carlinhos na lile la kusawazisha kwa Namungo kupitia kwa Stephen Sey.

Morroco amesema kuwa :"Ilikuwa ni mpira wenye ushindani mkubwa ndani ya uwanja ila haikuwa kazi rahisi wachezaji walipambana kusaka ushindi mwisho wa siku wakaambulia sare.

"Kukosa na kupata ni sehemu ya mchezo hivyo kwa sasa ambacho tunakifanya ni kupambana kwa ajili ya mechi zetu zijazo tayari mchezo wetu wa nyuma hatuwezi kubadili matokeo," amesema.

Pointi hiyo moja inaifanya Namungo ibaki nafasi tisa ikiwa na pointi 15 na Yanga pia inabaki nafasi ya pili ikiwa na pointi 25.