Jumapili , 24th Sep , 2017

Timu ya Azam FC inatarajiwa kushuka katika dimba lao la nyumbani Azam Complex, Chamazi Jiji la Dar es Salaam kuivaa Lipuli FC huku ikiwa na matarajio makubwa ya kuitoa kileleni Mtibwa Sugar katika msimamo wa Ligi ambao anaushikilia mpaka hivi sasa.

Akizungumzia mchezo huo Kocha Mkuu Aristica Cioaba amesema wamejipanga vizuri katika kuhakikisha wanachukua alama tatu katika mechi yao ya leo japo kuwa anatambua kila timu inawachezaji wazuri.

"Ninafuraha sana kuona wachezaji wanafanya mazoezi kwa nguvu na kusikiliza kila ninachotaka katika mechi hii dhidi ya Lipuli. Napenda kusema naheshimu kila timu hapa Tanzania kwa kuwa kila mmoja ana wachezaji wazuri lakini mipango yetu kwa leo ni kucheza soka zuri na kuchukua pointi tatu", alisema Cioaba.

Azam FC inashuka dimbani ikiwa na alama saba kibindoni ikiwa nyuma kwa pointi mbili alizokuwa nazo Mtibwa Sugar mpaka hivi sasa, ambapo naye Mtibwa Sugar atakuwa dimbani siku ya leo dhidi ya Ruvu Shooting FC akisaka alama tatu huku akimuombea njaa Azam FC asifunge ili aweze kubakia yeye nafasi ya juu.