Jumatano , 22nd Nov , 2017

Klabu ya soka ya Azam FC inayoshiriki ligi kuu soka Tanzania bara imeanza usajili kwa nguvu baada ya jioni ya leo kutangaza kumsajili mshambuliaji Bernard Arthur kutoka klabu ya Liberty Professional ya Ghana.

Arthur amesaini mkataba wa miaka miwili kujiunga na timu hiyo inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kuu. Mchezaji huyo ametambulishwa na Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdul Mohammed, ambaye alisafiri hadi nchini Ghana kukamilisha usajili huo.

Abdul ameeleza kuwa usajili wa Arthur mwenye  miaka 20, ni sehemu ya mapendekezo ya benchi la ufundi la timu hiyo kwenye usajili huu wa dirisha dogo ambalo limefunguliwa tangu Novemba 15 na litafungwa Desemba 15.

Arthur amekuja kuziba pengo la straika mwingine, Yahaya Mohammed, aliyeondoka baada ya mkataba wake kusitishwa kwa makubaliano maalumu ya pande mbili wiki chache zilizopita.