Jumapili , 19th Nov , 2017

Klabu ya soka ya Azam FC imeendelea kuwakaba koo vinara wa ligi kuu soka Tanzania bara Simba kwenye msimamo baada ya kuibuka na ushindi ugenini dhidi ya Njombe Mji. 

Azam FC imeibuka na ushindi wa bao 1-0 kwenye mchezo wake wa raundi ya 10 dhidi ya Njombe Mji uliomalizika jioni hii kwenye uwanja wa Sabasaba mjini Njombe. Bao pekee la Azam FC limefungwa na nahodha Aggrey Morris.

Kwa matokeo hayo Azam imeendelea kukimbizana na Simba kileleni kwa alama 22 ikizidiwa mabao ya kufunga hivyo kubaki katika nafasi ya pili ikifuatiwa na Yanga yenye alama 20.

Katika mchezo mwingine wa leo uliokamilisha raundi ya 10 umeshuhudiwa Mtibwa Sugar ikikubali kupoteza mchezo wake wa kwanza kwenye ligi kuu soka Tanzania bara msimu huu baada ya kuchapwa bao 1-0 na Kagera Sugar.

Bao la Kagera Sugar ambayo ilikuwa ugenini Manungu limefungwa na Edward Christopher. Matokeo hayo yanaifanya Mtibwa Sugar isalie katika nafasi ya nne ikiwa na alama 17 sawa na Singida United ambayo ina alama 17 pia.