Jumanne , 26th Sep , 2017

Klabu bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC inatarajiwa kuondoka kesho (Jumatano) jijini Dar es Salaam kuifuta Singida United katika mchezo wa Ligi Kuu, mzunguko wa tano utakaopigwa katika viunga vya Jamhuri Jijini Dodoma.

kikosi cha klabu bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC.

Mchezo huo unatarajiwa kufanyika Septemba 30 mwaka huu majira ya saa 10:00 jioni, huku Azam FC ikiwa ndiyo timu pekee mpaka sasa iliyoweza kulinda nyavu zake kutochunguliwa katika mechi zote nne za awali walizocheza katika viwanja mbalimbali.

Akizungumza Kocha Msaidizi wa Azam FC, Idd Nassor Cheche, amesema kuelekea mchezo huo wanatarajia kulifanyia kazi tatizo la ufungaji kwenye kikosi hicho baada ya kupoteza nafasi nyingi za wazi katika mchezo uliopita.

Kwa mujibu wa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Azam FC imeweza kushika nafasi ya pili kwa alama 10 ikiwa sawa na Mtibwa Sugar iliyo kileleni, ikizidiwa kwa tofauti ya mabao ya kufunga.