Jumatano , 24th Mei , 2017

Timu za Simba na Yanga zinatarajia kuwania shilingi milioni 60 za michuano mipya SportPesa Super Cup inayotarajiwa kutimua vumbi kuanzia Juni 5 katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam na kushirikisha jumla ya timu 8 kutoka Tanzania na Kenya

Simba na Yanga walipokutana msimu huu

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Utawala na Utekelezaji wa Kampuni ya SportPesa Tanzania, Tarimba Abbas ambaye amesema kuwa michuano hiyo itajumuisha timu nne kutoka Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar ambazo ni Simba SC, Yanga SC, Singida United na Jang'ombe Boys na upande wa Kenya ikiwa ni Gor Mahia, AFC Leopards, Nakuru All Stars pamoja na Tusker FC.

“Mashindano haya yatakuwa na siku 12 na yameshapata idhini kutoka TFF na tunashirikiana nao na tutaendelea kushirikiana nao lakini vilevile nalo Shirikisho la soka la Kenya wameyaruhusu hivyo tunaamini mashindano haya yatakuwa ya mfano na yatajaribu uwezo wa timu zetu zinapokutana na timu za nje, timu zitakazoshiriki mashindano haya ni zile zinazodhaminiwa na SportPesa Tanzania". Amesema Tarimba.

Aidha, Tarimba amesema mashindano hayo yatachezwa kwa mtindo wa mtoano ambapo kwa siku moja kutakuwa na mechi mbili na siku inayofuata zitapigwa hivyo hivyo, kisha itafuata nusu fainali na baadaye fainali.

Mkurugenzi wa Utawala na Utekelezaji wa Kampuni ya SportPesa Tanzania, Abbas Tarimba

Kuhusu waamuzi na fedha za maandalizi, Tarimba amesema "Watakuja waamuzi ambao siyo watanzania wala siyo wakenya lakini haina maana waamuzi wa nyumbani watakuwa wanakaa na kuangalia ili kuweza kukwepa lawama zinazotokana na waamuzi....Timu zote ambazo zitaingia kushiriki zitapatiwa fedha zaidi ya shilingi milioni 5 kwaajili ya ushiriki"

Amesema timu zitakazoingia nusu fainali zitapata zaidi ya shilingi milioni 10 kila moja na bingwa atapata zaidi ya shilingi milioni 60 huku mashindi wa pili akipata zaidi ya shilingi milioni 12

 Vituo vya Radio na TV vya kampuni ya IPP vinarajiwa kurusha matangazo ya mashindano hayo mubashara.

RATIBA YA SPORTPESA SUPER CUP

Juni 5, 2017
Singida United Vs FC Leopard
Yanga SC Vs Tusker FC

Juni 6, 2017
Jang`ombe Boys vs Gor Mahia
Simba Vs Nakuru All Star

NUSU FAINALI
Juni 8, 2017

Singida United/AFC Leopards Vs Yanga SC/Tusker FC
Simba SC/Nakuru All Star Vs Jangombe Boys/Gor Mahia

FAINALI
Juni 11, 2017

Msikilize hapa Tarimba akifafanua zaidi