Jumatatu , 31st Mei , 2021

Msanii wa Bongofleva Mwasiti, ambaye amekuwa akijihusisha kwa kiasi kikubwa na masuala ya kijamii ikiwemo mabinti, amesema moja ya changamoto aliyobaini ni wazazi kuwa mbali na watoto wao wa kike hivyo hata mambo ya hedhi salama hawayaongelei.

Msanii Mwasiti (kulia) akikabidhi mchango wake wa pedi kwa balozi wa Kampeni ya Namthamini Deogratius Kithama.

Mwasiti ameongea hayo kwenye uzinduzi wa Kampeni ya Namthamini 2021 ambayo ina lengo la kukusanya pedi kwaajili ya wanafunzi wa kike zaidi ya 5,000 nchini.

''Mimi nimezunguka sana Tanzania kwenye haya mambo ya watoto wa kike, kuna changamoto kubwa ya ukaribu baina ya wazazi na mtoto wa kike hususani anapofikia umri wa hedhi. Kutokana na umbali huo anakosa kuwa karibu na wazazi hivyo hata kuongelea hedhi salama inakuwa vigumu. Naomba huo mpaka uondolewe,'' ameeleza.

Tangu kampeni ya Namthamini NasimamaNaye ianze mwaka 2017, East Africa Television na East Africa Radio, zimefanikiwa kugawa pedi zaidi ya 40,000 ambazo zimewasaidia wanafunzi zaidi ya 10,000 nchini kote.