Jumatano , 20th Jan , 2021

Kampuni inayojihusisha na michezo ya kubahatisha ya Meridian Bet, imetoa msaada wa vitu mbalimbali kwa walemavu wanaosali katika kanisa la Waadiventista wasabato, Manzese Jijini Dar es Salaam.

Meneja Ustawi wa Kampuni ya Meridian Bet, Amani Maeda, akikabidhi msaada kwa mmoja wa walemavu jijini Dar es Salaam

Akizungumza wakati akitoa msaada huo Meneja Ustawi wa Kampuni hiyo Amani Maeda, amesema kuwa kampuni hiyo imejiwekea utaratibu wa kusaidia watu wenye uhitaji maalum ambapo leo wameamua kutoa msaada kwa taasisi hiyo.

"Huu ni mwendelezo wa kutoa msaada kwa watu wenye uhitaji maalum na hapa tumekuja na mchele, unga wa ugali, sukari, mafuta ya kupikia, pempas za wakubwa pamoja na miwani lakini mtatuambia changamoto mlizonazo ili kwenye mkono wa kugusa Jamii tuweze kuwafikia", amesema Amani Maeda.

Kwa upande wake mratibu wa walemavu hao Oloo Vincent, ameshukuru kwa msaada huo ambapo pia ametumia nafasi hiyo kuiomba serikali pamoja na jamii kwa ujumla kuwaunga mkono walemavu hao kwani pamoja na ulemavu walionao lakini wanajishughulisha na ushonaji wa viatu.

Nae Mwenyekiti wa walemavu hao Isdori Mrisho, ameishukuru kampuni hiyo kwa moyo wao wa utoaji na kuongeza  kuwa  watu wengi wana uwezo mzuri kiuchumi lakini hawana moyo wa utoaji.

Akizungumza kuhusiana na kuwakumbuka walemavu walioko vijijini, Katibu wa Walemavu hao Berdina Sailas, amesema kuwa asilimia kubwa ya walemavu wako vijijini na hawapati msaada kwa kuwa watu hawawafikii hivyo ameiomba kampuni ya Meridian Bet iangalie namna ya kuwafikia walemavu walioko vijijini.