Ijumaa , 28th Mei , 2021

Ikiwa leo ni Siku ya Hedhi Salama Duniani, East Africa Television na East Africa Radio imezindua kampeni ya Namthamini kwa mwaka 2021, tayari kwa kukusanya taulo za kike (pedi) na kuzigawa kwa wanafunzi wa kike wenye uhitaji waliokatika mazingira magumu katika maeneo mbalimbali nchini.

Balozi wa Kampeni ya Namthamini Deogratius Kithama akipokea mchango wa pedi kutoka kwa Devotha Mkwawa

Akiongea kupitia kipindi cha DADAZ ambapo uzinduzi umefanya rasmi mtangazaji wa kipindi hicho Bhoke ameeleza mafanikio makubwa ya kampeni hiyo ambayo kwa mara ya kwanza ilianza mwaka mnamo mwaka 2017.

Mtangazaji Bhoke

''Tangu kampeni ya Namthamini NasimamaNaye ianze mwaka 2017, East Africa Television na East Africa Radio zimefanikiwa kugawa pedi zaidi ya 40,000 ambazo zimewasaidia wanafunzi zaidi ya 10,000 nchini kote,'' ameeleza Bhoke.

Aidha, moja ya wazalishaji wa pedi ambao wamekuwa wakishirikiana na East Africa Television na East Africa Radio kwa kiasi kikubwa katika kufikia lengo, kampuni ya Keys Pads kupitia mwakilishi wake Heris Mtui wamesema kwa sasa suala la pedi lipo wazi zaidi ukimya umeshavunjwa.

Heris Mtui kutoka Keys Pads

''Unajua wakati kampeni ya Namthamini inaaza mambo hayakuwa kama leo, kiukweli tumefanikiwa sana kuvunja ukimya na hata dukani huwezi kukuta tena pedi zinafichwa badala yake zinawekwa kama bidhaa za mbele kabisa,'' amesema Mtui.

Msanii Madee ni miongoni mwa wageni kwenye uzinduzi wa Kampeni ya Namthamini