Alhamisi , 8th Dec , 2016

Serikali imesema shule zote zenye upungufu wa matundu ya vyoo, au zisizokuwa na vyoo zitafungwa endapo kasoro hiyo haitarekebishwa ndani ya mwaka mmoja.

Mwalimu wa Shule ya Msingi ya Kibirashi iliyopo Kilindi Mkoani Tanga akionesha choo cha muda cha shule hiyo.

 

kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Mhandisi Stella Manyanya alipokuwa akijibu maswali ya wananchi kupitia kipindi cha Kikaangoni kinaruka LIVE kupitia ukurasa wa Facebook wa EATV kila Jumatano saa 8:00 mchana.

Manyanya amesema wazazi na wananchi kwa ujumla wana jukumu la kujenga vyoo katika shule ambazo watoto wao wanasoma, hivyo wahamasishwe na kumaliza tatizo hilo ndani ya mwaka mmoja.

"Katika suala la vyoo, tumewaachia wazazi wawajibike, maana kama wameweza kujenga madarasa, watashindwaje kujenga vyoo?? tatizo hili haliko vijijini pekee yake, liko hadi mijini, nimetembelea shule kama Zanaki hapa Dar es Salaam, nimekuta hali mbaya sana, kwahiyo kuna mambo mengine tunaona ni lazima wananchi waendelee kusaidia maana ukiisubiri serikali inaweza ikachukua muda mrefu zaidi" Amesema Manyanya

Mhandisi Stella Manyanya

"Tumetoa mwaka mmoja, shule zote na hasa za serikali zitakazokuwa hazina matundu ya vyoo ya kutosha, na zile ambazo mazingira ya vyoo ni mabaya, tutazifunga bila ubaguzi wa shule ya serikali na binafsi"

Kuhusiana na ubovu wa miundombinu mingine ya shule, Manyanya amesema shule zaidi ya 81 tayari zimeanza kuboreshwa na kuwataka wadau wa maendeleo kusaidia kwa kuwa mwanafunzi asipokuwa kwenye mazingira bora, hawezi kupata elimu bora.

Tags: