Jumatatu , 12th Oct , 2015

Mashindano makubwa ya kucheza Afrika Mashariki ya Dance100% 2015 yaliyoratibiwa na East Africa Radio na East Africa Television, yamefikia kikomo chake jumamosi hii na kupatikana mshindi aliyejinyakulia kitita cha shilingi milioni 5 za Kitanzania.

Akiongea baada ya mashindano hayo kukamilika jaji mkuu wa shindano hilo Super Nyamwela, amesema ushindani ulikuwepo mwaka huu ni mkubwa, na kuonyesha kuwa mashindano hayo yamekuwa na kuleta changamoto nyingi.

"msimu wa nne wa mashindano haya ya Dance 100% yamezidi kuwa advanced, kwa sababu ukiangalia mashabiki, ukiangalia majumbani, ukiangalia East Africa nzima, hili shindano wanalifuatilia, ina maana kwamba tulivyoanzia mwaka wa nne leo mpaka kuja kufikia fainali hii, madancers wamezidi kuweka upinzani wa kweli,"alisema Super Nyamwela.

Super Nyamwela aliendelea kwa kuyafananisha mashindano hayo na timu pinzani za mpira wa miguu za Simba na Yanga, kutokana na changamoto zilizokuwepo ambazo amedai ndizo zilizoyapa umaarufu mashindano hayo.

"Kama ingekuwa timu za mpira tungefananisha na Simba na Yanga, wanachukiana kwa sababu ya upizani umekuwa uko juu sana, ambao inasababisha mashindano kuwa juu, wamejipanga kuweza kujua kuwa hii kazi ni kama kazi nyingine, na kazi ya dancers ina maana iko juu sana, kwa hiyo naweza nikazungumzia fainali za safari hii ni kubwa sana tofauti na tulikoanzia ", aliendelea kusema Super Nyamwela.

Nae Mkuu wa matukio kutoka Baraza la Sanaa Taifa (BASATA) Kurwigira Maregesi ambaye pia ni mmoja wa waratibu wa mashindano ya Dance100%2015, amewataka watu mbali mbali kujitokeza na kuinua vipaji vya sanaa, pamoja na kufanya kazi za sanaa wakifuata sheria.

"BASATA imekuwa mstari wa mbele kusapoti shughuli za sanaa ikiwemo na hii Dance100% na matukio mengine, tunashauri au tunasisitiza pia watu wengine wajitokeze kuinua vipaji vya Watanzania kwa namna moja au nyingine, na ushauri wangu mwengine ni kwamba tuharibu kufanya kazi za sanaa kwa mujibu wa taratibu na sheria zilizowekwa nchini", alisema Maregesi.

Kundi la WD ambalo limetokea Temeke jijini Dar es Salaam, limeyabwaga makundi mengine manne kujinyakulia ushindi huo, wakifuatiwa na kundi la Team ya shamba, na kundi la Best Boys kaka zao kuchukua nafasi ya Tatu.