Jumatatu , 11th Sep , 2017

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Nchini DCI Robert Boaz amemtaka dereva wa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kufika polisi kwa ajili ya mahojiano juu ya tukio la kupigwa risasi kwa kiongozi huyo ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA.

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Nchini DCI Robert Boaz

Mkurugenzi huyo amesema hayo leo wakati akifanya mahojiano na kipindi cha HOTMIX  ambapo amesema "Polisi inaendelea kumtaka dereva huyo kufika kwa ajili ya kuisaidia Polisi katika uchunguzi wa tukio hilo".

Hata hivyo kuhusiana na dereva huyo (Simon Bakari), Mwenyekiti wa (CHADEMA) Freeman Mbowe jana katika taarifa yake alisema kutokana na dereva huyo kushuhudia tukio la kutisha wameamua kumpeleka Nairobi ili kupatiwa huduma za kisaikolojia 

Akizungumzia muitikio wa viongozi na watendaji mbalimbali wanaoendelea kufika katika Jeshi hilo kwa ajili ya mahojiano baada ya kutajwa katika taarifa mbili za Kamati za Bunge zilizochunguza Sekta ya Madini ya Almasi na Tanzanite, DCI amekiri kuridhishwa.

DCI Boaz amesema viongozi hao wamekuwa wakifika kwenye  kikosi maalum cha upelelezi ambacho kimeundwa na vikosi vyote vya Upelelezi, na kuongeza kuwa wanaendelea kuhojiwa na kwa wale watakaobainika kuhusika watapelekwa Mahakamani.

Amesema viongozi hao pamoja na wengine watakaofika wataendelea kuhojiwa kufuatia amri ya Amiri Jeshi Mkuu na kufuatiwa na wito wa Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Simon Sirro aliyetaka viongozi hao kufika kwa ajili ya mahojiano baada ya kutajwa kwenye taarifa za kamati hizo mbili.