Jumatano , 15th Feb , 2017

Rapa Nay wa Mitego ambaye sasa anafanya vyema na wimbo wake wa mapenzi 'Sijiwezi' amefunguka na kusema kesho Alhamisi, Februari 16 anaachia kazi ambayo itakuja kuleta shida nyingine mjini.

Nay wa Mitego akiwa Kikaangoni

Akiongea kwenye kipindi cha KIKAANGONI kinachorushwa LIVE kupitia ukurasa wa facebook wa EATV, Nay wa Mitego amesema sasa ni wakati wake na ni muda wa kuwapa burudani wale mashabiki zake wa hip hop ambao wamemzoea kumuona Nay wa Mitego kwenye michano na kurekebisha watu tabia.

Akiielezea kazi hiyo aliyoipa jina la 'Muda Wetu' Nay wa Mitego amedai kuwa hivi sasa ni wakati wa wasanii fulani fulani kufunga vilago kabisa na kuondoka katika game kwani tayari huu siyo muda wao lakini pia hawatakiwi hata kujipanga upya bali wanatakiwa kuondoka kabisa.

Kuhusu kuwa na hofu ya kufungiwa na Baraza la Sanaa Tanzania BASATA, Nay amesema hafanyi kazi kwa kuihofia BASATA "Sifanyi muziki kwa kuangalia kama utafungiwa na basata au hautafungiwa"

Mbali na hilo Nay wa Mitego anasema katika maisha ya kawaida yeye amekuwa mwekezaji mzuri sana kwenye ardhi hivyo anatumia nafasi hiyo kujipanga na maisha yake ya baadaye kwa kuwekeza vya kutosha kupitia ardhi.