Alhamisi , 23rd Mar , 2017

Msanii Mrisho Mpoto amewaomba wanasiasa waachie ‘gap’ kidogo ili wasanii nao waweze kupata muda wa kutambulisha kazi zao za sanaa kwa jamii ambayo sasa imetekwa na upepo wa siasa.

Mrisho Mpoto

Hayo yameibuka kutokana na matukio makubwa ya kisiasa kila kukicha na baadhi ya wasanii wakiongozwa na Mpoto kuandika katika mitandao ya kijamii kuwataka wanasiasa wajaribu kidogo kupunguza kasi yao ili nao waweze kusikika.

“Mtu amewekeza hela nyingi na anajaribu, anakuta hakuna ‘gap’ kwenye soko kwa sababu macho, mawazo yote ya watu yamehamia katika siasa.  Kwa hiyo nikasema hii ni hatari kwasababu unaweza sema labda kesho, keshokutwa patatulia, mtondo, mtondogo patatulia, unaichukulia kama mzaha vile lakini sasa unaona kila kukicha kuna ‘breaking news’ kwa hiyo nikasema hapana tafadhari kidogo watupe ‘gap’ kidogo ili watu waweze kufanya ‘promotion’ za nyimbo zao”. Alisema Mrisho

Aidha msanii huyo amesema siyo kweli kwamba wanasiasa hawaelewi chochote wanachowafanya wasanii na watu wengine wanaotegemea upepo wa ‘promo’ katika kufanya na kutangaza kazi zao.

“Wanasiasa wenyewe wanajua leo tukiamshe kipi siyo kwamba hawajui wana-strategy kabisa kesho tuamshe hiki keshokutwa tuamshe kile”. Alisisitiza Mpoto

Vile vile Mjomba amesema kwa sababu wanamsikia anawaomba kidogo ‘slow down’ ili vijana wao waweze ku-boost kazi zao kwa sababu ‘investment’ kubwa wameweka katika hizo shughuli, muda pamoja na fedha.