Mr. T Touchez hawezi kuniangusha - Nay

Friday , 17th Feb , 2017

Msanii wa muziki wa hip hop bongo Emmanuel Elibariki a.k.a 'Nay wa Mitego' amesema hawezi kushuka kimuziki kwa kuachana na producer Mr. T Touchez na kusema kuwa hajawahi kuanguka katika muziki wake kutokana na maneno  ya watu wanaomuombea mabaya.

Amefunguka hayo wakati akijibu maswali ya watu katika kipindi cha KIKAANGONI kinachoruka LIVE kupitia ukurasa wa Facebook wa EATV ambapo kuwa walitoa maoni yao kuwa ameshuka kimuziki baada ya kuachana na aliyekuwa producer wake Mr. T Touchez.

Amesema kuwa hakuna mtu ambaye ana uwezo wa kubadilisha upepo wa muziki wake na kwamba yeye anamuamini Mungu wake ambaye anapatia riziki, na kuongeza kuwa hashangazwi na maneno hayo kwa kuwa huwa hana bahati ya kusemwa kwa mazuri pindi anapokuwa karibu na mtu na baadaye kuachana naye, iwe kimapenzi au kikazi.

"Siwezi kushuka kwa ajili ya maneno ya watu na mimi na kwa sababu mimi ninamuamini Mungu wa dunia yangu ambaye kila nikimuomba ananijibu kwa wakati. Pia mimi siyo msanii aliyedumaa hivyo hakuna mtu ambaye ana uwezo wa kubadilisha upepo wa muziki wangu. Si mnaona sijiwezi inakamata Top 10 vituo mbalimbali hivyo sijashuka kimuziki". Alisema Nay wa Mitego

Nay wa Mitego akiwa KIKAANGONI

Nay ameongeza kuwa katika kipindi chote alichokuwa akifanya kazi na Mr. T Touchez alikuwa akimthamini kama producer ambaye anastahili kufanya kazi katika mazingira mazuri ndiyo maana hata kazi nyingine zilizokuwa zikifanyika katika studio yake ya Free Nation hakuwahi kumdai pesa yoyote ya kazi hizo.

 Aidha Nay ameeleza kuwa hana kinyongo na producer wake huyo ambaye walikwaruzana zaidi ya miezi sita iliyopita huku akiwa amegoma kueleza chanzo cha ugomvi wao na producer huyo aliyemuandalia 'hits' kadhaa.

"Sina kinyongo na Mr.T Touchez hata kidogo nipo tayari kufanya naye kazi kama akisema kwa sababu siwezi kuishi kwa kulipiziana visasi, na wala siwezi kujibizana naye, maana baba hawezi kujibiana na mtoto" alisema Nay.