Jumatatu , 24th Jul , 2017

Mtayarishaji wa muziki King Lufa amewataka wasanii kutoka 'Switcher Music Group' kuheshimu kipaji chake na kuwafahamisha kuwa muziki ni biashara kama zilivyo nyinginezo.

Lufa amelazimika kutoa kauli hiyo kwa madai ya kuwa kundi hilo limetoa nyimbo tatu alizozitengeneza wakati akifanya kazi kwenye studio ya switch na kusema kwamba anashangaa kazi zake kutoka bila makubaliano yoyote.

"Mimi muziki ni kazi yangu, na huwa sikubaliani na watu wanaotaka kunirudisha nyuma. Ni kweli mimi sasa hivi nipo Wanene lakini kuna kazi zangu nyingi niliziacha kwa Switcher nilioondoka cha kushangaza wanaendelea kutoa kazi nilizozitengeneza mimi. Wao wanazidi kunufaika kimuziki Halafu mwenye midundo sina taarifa siyo busara," alifunguka

Ameongeza kuwa "Sasa hivi nafanya biashara hakuna tena ile kupeana kazi kiushkaji. Hata kama kuna ugomvi hayo ni mambo yanayokujaga na kupita, kila moja aheshimu kazi ya mwenzake kwa sababu mwisho wa siku mimi na wao tunategemeana kwani hakuna msanii bila prodyuza. Tusichukuliane poa," aliongeza Lufa.

Kuachana na hayo mtayarishaji huyo nyimbo kubwa mbalimbali hapa nchini amewataka wasanii kuhakikisha wanajiongeza kutoka sehemu moja kwenda nyingine haswa wanapokuwa wakifanya shoo na kutotegemea kuimba kwa kutumia CD.

"Wasanii wetu wajiongeze, wao ndiyo watu wanaoutangaza muziki wa Tanzania hivyo ni vizuri wakabadilisha mifumo ya kufanya show, waanze kuimba hata 'Live' ili kupambana na wenzetu waliopiga hatua kimuziki. Wapige mazoezi ya kutosha," amesema