Jumapili , 13th Aug , 2017

Mtunzi wa vitabu mashuhuri Tanzania Erick James Shigongo, anatarajia kurudi shule na kusoma elimu ya shahada, baada ya kuhangaika muda mrefu kutafuta nafasi hiyo, huku akisukumwa na masimango na matusi ya mitandaoni.

Erick Shigongo

Kwenye ukurasa wake wa facebook Erick Shigongo ameandika waraka mrefu akielezea safari yake kitaaluma na furaha aliyonayo, ya kuweza kufikia ndoto yake ya kuwa na elimu ya chuo kikuu, licha ya kuwa na mafanikio makubwa kwenye kazi zake za utunzi na maisha kiujumla.

"Ndoto imetimia, hatimaye naingia Chuo Kikuu, nikiwa mtoto nilitamani sana kusoma hadi chuo kikuu lakini sababu ya umasikini na mazingira magumu hasa shule nilizosoma, sikufaulu mtihani wa darasa la saba, nikarudia darasa la saba katika shule nyingine lakini bado sikufaulu, nilijiona mjinga! Nikajaribu kupitia njia ya 'vikozi' vidogo ili hatimaye niingie chuo kikuu lakini sikufanikiwa, nikaachana na ndoto hiyo na kuanza ujasiriamali", aliandika Erick Shigongo.

Erick Shigongo alendelea kuandika akisema kuwa ndoto yake hiyo imefanikiwa baada ya kujiunga na mfumo wa RPL ambao walifanya watu wenye uzoefu auwaliofanya mambo fulani katika jamii bila kuwa na elimu, na kuwapa nafasi ya kusoma elimu ya juu, ndipo alifanikiwa kupata mwaka huu, baada ya mwaka jana kufeli.

"Nikakusanya vitabu vyangu ambavyo nimekwishaandika na kuvipeleke Tume ya Vyuo Vikuu na kuomba niruhusiwe kufanya mtihani huo, nikaruhusiwa, mwaka jana nikafanya na kufeli, sikukata tamaa, mwaka huu nikafanya tena na kufaulu, hivyo mwezi wa tisa ninaanza mwaka wa kwanza ", aliandika Erick Shigongo.

 

Alichokiandika Shigongo kwenye ukurasa wake wa facebook