Ijumaa , 18th Aug , 2017

Mwanamuziki mkongwe wa bongo fleva 'Prince Dully Sykes' Mr. Misifa' amefunguka leo mapya na kudai familia yake ilihusika katika kuleta uhuru wa nchi hii ingawa serikali imekuwa haiwakumbuki watu hao.

Akiwa kwenye Heshima ya Bongo Fleva ndani ya Planet Bongo ya EATV Dully amesema historia ya uhuru watu wengi wamekuwa hawaifahamu kwa kuwa serikali imekuwa haina tabia ya kuwakumbuka watu waliopambana kuleta uhuru.

"Babu yangu mimi alishiriki kikamilifu katika kuhakikisha nchi inapata uhuru. Lakini ndiyo hivyo serikali yetu huwa haiwakumbukagi hao watu. Mfano mimi babu yangu amefanya mengi hadi uhuru ukapatika, ni kati ya wale watu waliojichanga na kumpatia Mwalimu  Nyerere pesa aende kwa Waingereza kuomba uhuru. Siongei kama kutaka sifa, labda babu yangu watu hawamjui lakini hata historia ya mtu  aliyetunga wimbo wataifa naye hatumjui. Mimi babu alikataa kuwa Mwenyekiti wa TANU akamuachia Nyerere ambaye alikuwa rafiki yake sana," Dully alifunguka.

Hata hivyo Dully ameeleza sababu ya familia yake kushindwa kujitangaza mbele za watu kama ni watu waliopigania uhuru

"Familia yangu mimi siyo watu wa kuzungumza au kutaka kujionyesha sana, Mfano kama mimi watu wengi wanashindwa kunipa sifa zangu kwamba ndiye mwanzilishi wa bongo fleva zaidi ya nyinyi wachache ndiyo mmekuwa mkiisema hiyo itakuja kuwa babu yangu ambaye hajulikani? Ila ni vyema historia hizi watanzania wakapatiwa na kuijua historia ya nchi yao"