Jumanne , 10th Jan , 2017

Msanii wa muziki wa bongo fleva Lameck Ditto ambaye kwa sasa anafanya vyema na wimbo wake 'Moyo sukuma damu' amefunguka na kuwashauri vijana pamoja na wasanii kujifunza kutoka na kwenda kutafuta kazi.

Lameck Ditto

Amesema kusubiri kazi inaweza kuchukua muda mrefu kuipata na pia utakuwa unajifunga fursa nyingine ambazo huenda zinasubiri jitihada yako tu ili zifunguke.

Ditto amesema hayo kwenye kipindi cha Planet Bongo cha EATV na kusema hakuna mtu anaweza kukutafuta ili akupe kazi bali unatakiwa kujituma kutafuta kazi ili kupata kazi hiyo.

"Dunia ya sasa imebadilika hukuna mtu anaweza kukufuata ili akupe kazi ila inatakiwa kutoka na kwenda kuitafuta kazi, hata kwa wasanii wanatakiwa kutambua kuwa muziki saizi ni kazi na biashara hivyo wanapaswa kuwa na uongozi ambao utakuwa na kazi ya kutafuta kazi kwa ajili ya msanii huyo. Msanii saizi kusema umekaa tu unasubiri kazi zije unaweza kupata kazi mbili wakati huenda ungezitafuta kazi hizo ungepata kazi zaidi ya 20 ambazo zote unakuta zilikuwa zinakusubiri wewe". Alisema Ditto 

"Mfano sisi wasanii kuna makampuni unakuta yanataka kukutana na msanii fulani lakini yanashindwa kumpata huyo msanii, hivyo wasanii wasisubiri mpaka wafuatwe na makampuni bali wanatakiwa wao kuyatafuta hayo makampuni na kufanya nao kazi" alisema Lameck Ditto 

Suala la vijana kufanya kazi limekuwa likisisitizwa zaidi na Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli, na hatua hii ya Ditto inaamanisha kuwa msanii huyo ameanza kuimba wimbo ambao umekuwa ukiimbwa na Rais Magufuli