Jumanne , 25th Jul , 2017

Naibu Waziri wa Afya, Mh. Hamisi Kigwangalla ameahidi kuwafutia leseni, kuwanyang'anya vyeti na kuwafikisha kwenye mikono ya sheria watumishi wa sekta ya afya wenye tabia ya kuiba dawa na kwenda kuuza sehemu nyingine.

Mh. Kigwangalla ametoa ahadi hiyo leo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Itigi mkoani Singida kwenye ziara ya Rais Magufuli ya kuzindua miradi mbalimbali, ambapo Dkt. Kigwangalla amemshukuru rais kufanya maboresho makubwa katika sekta ya afya na kumuahidi tatizo la kuibiwa dawa hospitalini halitakuwepo tena.

"Wananchi hawatakosa dawa tena pindi watakapokwenda kwenye vituo vya afya vya Umma hapa nchini. Jambo la ukosefu wa dawa lilikugusa sana kipindi cha kampeni nakuahidi dawa ulizotupatia hazitaibiwa tena na niweke wazi kwamba mtumishi atakayethubutu kufanya hivyo nyundo nzito itamuangukia. Ukiachana na kwamba tutamfukuza kazini lakini pia tutamnyang'anya leseni yake pamoja na cheti ili asifanikiwe popote na baada ya hapo tutampeleka kwenye mikono ya sheria ilia ashitakiwe kwa makosa ya jinai kwani uwizi wa dawa ni sawa ni uwizi mwingine," Kigwangalla.

Hata hivyo Mh. Kigwangalla ameongeza kwamba kwa sasa bado wanashughulika na wauguzi wenye kauli chafu dhidi ya wagonjwa ili kuikomesha kabisa tabia hiyo.

"Ili kukomesha kabisa lugha chafu wanazozitoa baadhi ya wahudumu wa afya tumewataka kuweka na rekodi ya kila mzazi aliyepoteza mtoto ili tujue hayo matukio yanasababishwa na nini," aliongeza

Pamoja na hayo Naibu Waziri ameshukuru  Rais Magufuli kuboresha vituo vya afya kama vyumba vya upasuaji ambavyo vitasaidia changamoto zitokanazo na uzazi.