Jumatatu , 21st Aug , 2017

Mkuu wa wilaya ya Ubungo jijini Dar es salaam, Mh. Kisare Makori amefuta tozo mpya ya mabasi ya kusafirisha abiria, iliyowekwa na uongozi wa kituo cha mabasi cha Simu 200 maarufu kama mawasiliano.

Taarifa hiyo imetolewa leo alipoenda kusikiliza malalamiko ya madereva wa mabasi hayo ambao waliweka mgomo wa kusafirisha abiria mpaka pale watakaposikilizwa.

Mgomo huo ulioanza leo asubuhi uliwekwa baada ya madereva kukataa tozo mpya ya shilingi 1000 waliyoambiwa waanze kulipa, badala ya shilingi 500 ambayo walikuwa wakitoa awali kituoni hapo.

Pia madereva hao waligomea kulipa tozo hiyo iliyoongezwa bila kuboreshwa kwa huduma kituoni hapo, ikiwemo kurekebishwa kwa barabara inayotoka Sam Nujoma kwenda Mawasiliano, ambayo imekuwa ikilalamikiwa kwa ubovu na kuharibu magari yao.

Wakati huo huo Mkurugenzi wa Manspaa ya Ubungo Mh. John Lipesi Kayombo, amewaahidi madereva hao kuanza kushughulikia kero zao ikiwemo kureebishwa kwa hiyo barabara, pamoja na kero zingine ndogo ndogo ikiwemo huduma za vyoo na gharama zisizo eleweka ni za nini.