Jumapili , 23rd Jul , 2017

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewahakikishia wananchi wa wilaya ya Ileje kwamba serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara ya Mpemba-Isongole yenye urefu wa kilomita 58 na kuwajulisha kuwa itawapa fursa za kiuchumi na kupunguza kero ya usafiri.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na watumishi wa umma, viongozi wa dini na viongozi wa taasisi binafsi mjini Ileje hapo jana

Hayo yamesemwa na Mhe. Majaliwa jana jioni alipokuwa akizungumza na wananchi wa wilaya ya Ileje kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Stendi na kusema kwamba barabara hiyo itawawezesha wananchi wa wilaya ya Ileje mkoani Songwe, ambao wana mazao mengi kuyafikia masoko kwa urahisi.

“Ujenzi wa barabara hiyo utaongeza fursa za kiuchumi katika Wilaya ya Ileje,  hasa kufungua biashara za mipakani kati ya nchi ya Tanzania na Malawi.”

Pamoja na hayo Mhe. Majaliwa ameongeza kwamba serikali imedhamiria kuwaondolea wananchi changamoto mbalimbali hasa miundombinu ya barabara, hivyo aliwaomba waendelee kuiamini na kushirikiana nayo.