Jumapili , 19th Mar , 2017

Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo amewatoa hofu wananchi wa Zanzibar kuwa hawatakatiwa umeme baada ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuanza kulipa deni inalodaiwa na TANESCO.

Waziri wa Nishati na Madini, Prof Sospeter Muhongo

Prof. Muhongo amesema tayari SMZ imeanza kulipa kiasi cha Shilingi Bilioni 10 na itaendelea kulipa deni hilo mpaka litakapomalizika.

Aidha, Prof. Muhongo ametoa wito kwa wadaiwa sugu wote wa TANESCO kulipa madeni yao katika kipindi cha siku 5 zilizobaki kwa kuwa wasipolipa watakatiwa umeme. 

Taarifa hiyo ya Prof Muhongo imetoka baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, leo kukutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Waziri Muhongo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mhandisi Kahitwa Bishaija na Meneja Mwandamizi wa Fedha wa TANESCO Bw. Sadock Mugendi.