Jumatano , 15th Nov , 2017

Mganga Mkuu wa serikali Prof. Muhammad Bakar amekanusha juu ya dawa kinga zinazotolewa kwa wananchi na Wizara ya Afya kwa lengo la kuwakinga na magonjwa yasiyopewa kipaumbele kuwa zina madhara kama ambavyo imekuwa ikidaiwa na baadhi ya wananchi.

Prof. Bakar ameyasema hayo katika mkutano na wahariri wa vyombo vya habari na watumishi mbalimbali kutoka wizara ya afya jijini Dar es Salaam juu ya magonjwa yasiyopewa kipaumbele kama Matende, Mabusha,Usubi na Trakoma ambapo amewatoa hofu wananchi kuwa dawa hizo hazina madhara na mpaka sasa wamefanikiwa kupunguza kasi ya maambukizi ya magonjwa hayo mpaka asilimia 77 kwa baadhi ya magonjwa.

Dawa hizi hugawiwa bure na wizara ya afya kupitia mpango wa taifa wa kudhibiti magonjwa yasiyopewa kipaumbele ambapo awamu ijayo dawa zitaanza kugawiwa katika mkoa wa Dar es Salaam wananchi zaidi ya milioni nne wakitarajiwa kupatiwa dawa hizo, huku mwitikio mdogo wa wananchi hasa wa mijini ukitajwa kuwa changamoto kubwa katika mazoezi yaliyopita.