Jumatatu , 25th Sep , 2017

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari-TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko amethibitisha kukamatwa kwa boti iliyokuwa ikitumika kuiba mafuta kwenye bomba la  mafuta kwenye kina kirefu cha Bahari ya Hindi.

Mhandisi Kakoko ameyasema hayo Septemba 24 mbele ya Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango alipotembelea bandarini hapo ili kupata maelezo kuhusu mchakato wa kupata mita mpya za kupimia mafuta (Flow Meters).

Kakoko amesema kikosi maalumu cha kuzuia uhalifu cha Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) kimenasa wahalifu wakijiandaa kutoboa bomba na kuiba mafuta kwenye kina kirefu cha Bahari ya Hindi.

Waziri Mpango  amewapongeza askari wa doria waliofanikisha kukamata boti moja pamoja na vifaa vyake ikiwemo injini baada ya kuwadhibiti maharamia waliotaka kutoboa bomba na kuiba mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam.