Jumatatu , 16th Jan , 2017

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba amefunguka na kumjibu mbunge wa Kigoma Mjini Mhe. Zitto Kabwe kuhusu hali ya chakula nchini na kusema kuwa alikurupuka kwani kile alichokisema hakina ukweli wowote

Dkt. Tizeba (Kushoto) , Zitto Kabwe (Kulia)

Waziri Tizeba amesema kuwa nchi ilikuwa na chakula cha kutosha hivyo hakukuwa na haja ya NFRA kuongeza chakula kingine kwani kulikuwa na ziada ya chakula tani milioni tatu.

"Yupo mtu mwingine alikurupuka na kusema jamanii Tanzania imebakiza chakula cha siku nane, sasa hivi ni wiki ya tatu inakwenda ya nne watu bado wanakula, na hatujatoa chakula huko NRFA hata kilo moja, harafu nisemee suala la kuwa na akiba ya tani 90,000  hii nchi ina mavuno makubwa ina ziada ya tani milioni tatu hivyo kwanini NRFA wakanunue tani zingine milioni moja ili iweje. Tulikuwa na tani zaidi ya milioni tatu za ziada NRFA wangeenda kununua tani elfu moja au elfu tisini au laki tatu za nini? Alihoji Waziri wa Kilimo 

Mbunge wa Kigoma Mjini kupitia tiketi ya ACT Wazalendo Mhe. Zitto Kabwe mnamo tarehe 3 ya mwezi Januari kupitia ukurasa wake wa Facebook alitoa taarifa juu ya hali ya chakula nchini na kusema chakula ambacho kilikuwepo kwenye ghala ya Taifa ya chakula kilikuwa ni chakula cha kutosha siku nane tu pekee.

Mbunge huyo alikwenda mbali zaidi na kusema kwa mujibu wa taarifa ya Benki Kuu (BOT) ya mwezi Novemba 2016 ilionesha kuwa ghala la Taifa la chakula NFRA lilibakiwa na tani 90,000 tu za chakula.

"Ghala la Taifa lina hifadhi ya chakula kinachotosha siku 8 tu ikitokea dharura yeyote. Novemba 2015 kulikuwa na chakula cha kutosha miezi 2. Taarifa ya Benki Kuu ya mwezi Novemba inaonyesha kuwa NFRA imebaki na tani 90,000 tu za chakula". Aliandika Zitto Kabwe