Alhamisi , 25th Aug , 2016

Naibu mwanasheria mkuu wa Serikali, Gerson Mdemu amewataka watumishi wanaofanya kazi kwenye ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali kufanyakazi kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu ili kuifanya ofisi hiyo kuwa ya mfano mzuri wa kuigwa.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. George Mcheche Masaju .

Mdemu ametoa kauli hiyo wakati akifungua mafunzo ya uongozi ya kuwajengea uwezo mawakili na waendesha mashtaka wa serikali nchini yaliyofanyika katika ukumbi wa hazina mjini hapa.

Amesema watumishi hao ni lazima wafuate kanuni na maadili ya viongozi wa umma wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao ya kila siku ikiwa ni pamoja na kutunza siri na viapo vyao.

“Mafunzo hayo yakawe chachu ya kuwawezesha kukabiliana na changamoto mbalimbali mnazokabiliana nazo katika kutekeleza majukumu yenu ya kila siku,” alisema Mdemu.

Naye Neema Mwanda ambaye ni wakili mfawidhi wa serikali kutoka Mkoani Kilimanjaro amesema kuwa changamoto kubwa inayowakabili ni aina za uhalifu na watu wanaofanya uhalifu huo nchini.

Amesema kila kukicha nchini kuna aina mbalimbali za uhalifu unaotokea na kufanywa na watu tofauti tofauti hivyo kuleta changamoto kubwa kwao namna ya kukabiliana na kesi za aina hiyo.

Kwa upande wake wakili mfawidhi mkuu kutoka mkoani Mbeya Joseph Pande, amesema kuwa wana wajibu mkubwa wa kuwasimamia mawakili wa serikali katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku bila kupendelea mtu au kundi lolote.

Amesema ili mawakili na wanasheria wa serikali waweze kutekeleza majukumu yao ya kila siku ni lazima wafuate kanuni, sheria na utaratibu na miongozo iliyopo ili waweze kutenda haki katika kazi zao.