Ijumaa , 24th Apr , 2015

Watanzania wametakiwa kuwa waangalifu kwenye matumizi ya teknolojia ya mitandao ya kijamii ili wasiweze kuingia kwenye matatizo na mamlaka za kisheria.

Maria Sasabo (mwenye kofia) akimueleza jambo mkuu wa mkoa wa Njombe Rehema Nchimbi (kushoto).

Wito huo umetolewa leo na meneja wa mamlaka ya mawasiliano nchini (TCRA) kanda ya kati Maria Sasabo wakati akizungumza na East Afrika Radio ofisini kwake mjini Dodoma.

Sasabo amesema baadhi ya watu nchini wamekuwa wakiitumia vibaya mitandao ya kijamii kwa kuwatapeli watu hali ambayo huwafanya wengi wao kuishia mikononi mwa vyombo vya dola.

Alisema teknolojia ya mawasialino imeletwa ili kuwarahisishia watu mawasiliano nchini pamoja na ulimwenguni kwa ujumla lakini kuna baadhi ya watu wamekuwa wakiitumia kinyume kwa ajili ya kuwatapeli watu wengine.

Kwa upande wake mhandisi Charles Ambele kutoka mamlaka ya mawasiliano kanda ya kati amewatahadharisha watanzania kutoweka taarifa zao muhimu wakati wa kujiunga na mitandao ya kijamii kwani mara nyingi wahalifu wa mitandao hutumia taarifa hizo kuwatapeli watu husika.