Jumanne , 27th Sep , 2016

Mwanaharakati wa kupinga ndoa za utotoni nchini Tanzania Rebeca Gyumi amewataka vijana ambao wamepata nafasi ya kusoma na kupata elimu, kukumbuka kuisaidia jamii katika mambo yanayowakwamisha kimaisha.

Mwanaharakati Rebeca Gyumi akionesha tuzo aliyopewa na UNICEF akiwa katika studio za EA Radio

Rebeca ambaye pia ni Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali, Msichana Initiative linalotetea haki za wasichana kupata elimu, ameshinda tuzo ya Umoja wa Mataifa inayotolewa kupitia UNICEF katika kipengele cha mabadiliko ya kijamii.

Ametoa ujumbe huo alipokuwa katika kipindi cha SUPAMIX alipokuwa akielezea namna ambavyo ameweza kutambulika na kupewa tuzo na shirika la UNICEF kupitia Umoja wa Mataifa.

“Hakuna kitu kizuri kwangu kama kutumia elimu yangu kusaidia jamii ambayo nimeilelewa, mimi ni zao la jamii kuona kwamba elimu niliyopata kuna watu walijinyima ili mimi niweze kusoma, ndiyo maana natumia nilichokipata kuweza kurudisha angalau fadhila za jamii yangu” Amesema Gyumi.

Rebecca ameongeza kuwa ni vyema viongozi ndani ya jamii yetu wakiwafundisha vijana namna ya kuitumikia jamiii yetu kuliko vijana wa kitanzania kufundishwa na mataifa mengine juu ya namna ya kuwa kiongozi bora ndani ya jamiii kwa kuwa jamii ya kitanzania itaendelezwa na watanzania wenyewe .

Kutokana na ujasiri aliouonesha wa kufungua kesi dhidi ya serikali kuhusu sheria ya ndoa iliyokuwa inatoa fursa kwa mabinti wadogo kuolewa ndipo UNICEF ikaweza kumtunuku tuzo ya kutambua mchango wake, shughuli ambayo ilifanyika nchini Marekani.