Alhamisi , 17th Sep , 2020

Wanataaluma wote wa sekta ya afya nchini wametakiwa wawe wamejisajili, na kuhuisha leseni kwenye mabaraza yao ya kitaalam ndani ya miezi sita kuanzia sasa na wale ambao wamejiendeleza zaidi kitalaamu wanatakiwa kuhuisha (update) vyeti vyao vya viwango katika mabaraza ili kutambulika.

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi pichani.

Rai hiyo imetolewa leo na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi wakati akiongea na wasajili wa mabaraza mbalimbali ya kitaalam ya Wizara ya Afya pamoja na wasajili wa bodi zilizo chini ya wizara hiyo.

“Kila mwanataaluma aliyemaliza mafunzo yake ni vizuri awe amesajiliwa katika mabaraza yao, agizo hili ni kwa wanataaluma wote katika sekta ya afya ili muweze kutambulika, na uzuri hivi sasa kuna tovuti hivyo mnaweza kupata kujisali , kulipia na baadae kutumiwa  vyeti vyenu bila kuchelewa.  Kwa mantiki hiyo nawapa miezi sita wawe wamesajiliwa”. Alisisitiza

Pia wanatataaluma wanaojiendelea kwa ngazi mbalimbali ya taalauma ya afya kama uzamili na uzamivu 'PhD’ wanatakiwa kusajili hivi viwango katika mabaraza yao ili watambulike.

Prof. Makubi amesema utaratibu huo umewekwa na serikali kupitia mabaraza hayo hivyo kila mwana taaluma anatakiwa kujisajili au kuhuisha leseni ambazo zimeisha muda ili waendelee kutambulika na kufanya kazi zao.

Aidha,Prof. Makubi ameongeza kuwa wizara kupitia mabaraza hayo imeweka miundombinu ya mafunzo endelevu ya kitaaluma kwa kila taaluma kwa kufanya mitihani kwa ngazi zote."Lakini mtu aliyefanya mtihani nje ya utaratibu huu basi anatakiwa kuleta  ili kufanya usajili ili kupata alama na uwekwe kwenye kiwango stahili na ndio utaonekana bado upo kwenye kiwango cha uelewa kwenye taaluma yako na kuwatumikia wananchi”.

Kwa upande wa baadhi ya watu wa sekta ya afya wanaojipa hadhi ya kiwango fulani cha taaluma bila ya kujisajili kwenye mabaraza ya kitaaluma, Prof. Makubi ametoa miezi mitatu kwa wale wanataaluma wenye vyeti vyao wajisajilii ili kutambulika wapo katika kiwango fulani cha taaluma.

“Kuna baadhi ya wataaluma wanaojipa hadhi ya kiwango fulani cha kitaaluma wakati hawajasajili vyeti vyao  kwenye mabaraza, nitoe mfano kuna wanataaluma wanaojiita mabingwa wa kitu fulani (specialist, consultant ) na wanajitangaza kwa wananchi wakati hatuna ushahidi na kumbukumbu. Kwahiyo tumekubaliana na mabaraza suala hilo sasa lifikie mwisho na wote waliojiendeleza zaidi waje wajisajili haraka kwa kuwasilisha vyeti vyao.” Alisisitiza Prof. Makubi.

Hata hivyo Mganga Mkuu wa Serikali aliwaagiza waganga wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi wa Hsopitali, taasisi za afya, vyuo vya afya na waganga wafawidhi wote kuzingatia kusimamia utekelezaji wa maagizo haya kwenye sekta zote za afya ili kulinda viwango na hadhi ya taaluma husika. “Taaluma zote za afya lazima ziendelee kuheshimika na kusimamiwa vizuri ili kulinda afya za wananchi kwa viwango vya juu na bila kuruhusu wanataaluma bubu”, Alisema Prof Makubi.

Pia kwa Waganga wa tiba asili wametakiwa kufuata utaratibu wa kujisajili pamoja na wasaidizi wao na kufuata miongozo ya utoaji wa tiba asili na tiba mbadala kwani serikali ipo tayari kuwapa ushirikiano kwa kuwasaidia malengo yao ya utoaji wa tiba asili yanafanikiwa.