Jumatano , 24th Mei , 2017

Mbunge wa jimbo la Rufiji, Mohamed Mchengerwa (CCM) amefunguka na kusema kuwa katika bunge hili la 11, kuna wabunge watatu ambao wanaishi maisha magumu sawa na wananchi wao na kwamba wamekondeana kutokana na ugumu huo wa maisha.

Mohamed Mchengerwa - Mbunge wa Rufiji

Mchengerwa amewataja wabunge hao kuwa ni pamoja na Mbunge wa Mkuranga Abdallah Ulega, Mbunge wa Kibiti Allya Seif Ugando na yeye mwenyewe Mbunge wa Rufiji na kuongeza kuwa ugumu ho wa maisha unachangiwa na tatizo la mauaji yanayoendelea katika maeneo hayo.

“Mheshimiwa Mwenyekiti nataka nikuhakikishie katika Bunge lako hili tukufu unao wabunge watatu ambao wanaishi katika maisha magumu sana kupata kutokea katika nchi hii, Mbunge wa Mkuranga, Mbunge wa Kibiti pamoja na Mbunge wa Rufiji tunaishi katika maisha magumu siyo sisi tu hata familia zetu lakini pia hata wapiga kura wetu wanaishi maisha magumu sana wananchi wamekonda mpaka wanashindwa kushiriki katika shughuli za maendeleo, na tunaiomba serikali jambo hili ilifanyie kazi haraka sana" alisema Mchengerwa 

Mbali na hilo Mchengerwa ameiomba serikali kuwa sikivu huku akitaka Rais Magufuli atambue kuwa mambo yanayoendelea Pwani hayatokei kwa bahati mbaya, bali mambo hayo yana vyanzo vyake na hupangwa.

"Mambo haya yanayoendelea Kibiti, Rufiji na Mkuranga ni mambo yaliyopangwa na yana root course tunataka serikali ijue hilo, yapo mambo mengi na ziko chuki nyingi ambazo zimejengwa kwa wananchi, zipo chuki nyingi ambazo zilifanyika yanatoa kero kubwa kwa wananchi, jambo hili ni kubwa na linaendelea kutanuka kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine hivyo serikali inapaswa kuchukua hatua sasa" alisistiza Mchengerwa